angalia mikasa ya Mtoto wa MTAANI hapa |
Takwimu zinazoonyesha kuwa
watoto milioni 2.5 wamekuwa yatima baada ya wazazi wao kufariki dunia
kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na wakati huohuo, watoto wa kike watatu
kati ya 10 wamebainika kufanyiwa ukatili wa kingono kabla ya kufikisha
miaka 18.Hakika, idadi hii ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu inatisha. Sisi tunaona kwamba sasa kuna kila sababu kwa serikali na jamii nzima kutafuta namna bora ya kuwasaidia watoto hawa kwani vinginevyo, athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa taifa kuliko inavyoweza kudhaniwa.
Ninakumbushia hili huku nikijua kwamba hivi sasa, zipo jitihada kadhaa zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la kuongezeka kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi.
Kwa mfano, tunajua kuwa hadi sasa, serikali imekuwa ikijenga uwezo wa kitaalamu kwa maofisa wa ustawi wa jamii, kuanzisha na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, kukusanya takwimu za watoto hao na pia kutoa msaada wa kisheria kwa watoto.
Ni ukweli kwamba athari za kuwapo kwa watoto wanaoshi katika mazingira hatarishi ni kubwa kwa taifa na hivyo, wakati jitihada za kukabiliana na visababishi vya kuwapo kwa watoto hao zikiendelea kufanywa, upo ulazima pia wa kuhakikisha kwamba watoto hawa waliopo mitaani wanapatiwa upendo na huduma zote kama ilivyo watoto wengine.
Ikumbukwe kuwa, ikiwa watoto wa mitaani wataendelea kuachwa wajitafutie wenyewe maisha yao, ni dhahiri kwamba nao hawatakuwa na upendo kwa jamii inayowazunguka pindi watakapokuwa watu wazima.
Halitakuwa jambo la kushangaza kuona kuwa watoto hawa, baadaye ndiyo wanaokuwa sehemu ya watu hatari kwa ujambazi katika jamii. Haitashangaza pia kuona baadaye kuwa watoto hao wasiopata malezi bora wakiishia kuwa kina 'dada poa' wanaouza miili yao katika klabu za usiku na hivyo kuongeza kasi ya maambukizi ya ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa nchini.
chanzo JamiiForums 2015
No comments:
Post a Comment